USISUBIRI MWISHO WA MWAKA KUANZA MABADILIKO – DKT. LEKASHINGO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 9, 2026

USISUBIRI MWISHO WA MWAKA KUANZA MABADILIKO – DKT. LEKASHINGO



Na Mwandishi Wetu - DODOMA


Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, amewahimiza watumishi wanawake wa Tume kuanza kuchukua hatua za kufanya mabadiliko chanya katika maisha yao sasa, badala ya kusubiri mwisho wa mwaka ndipo waweke mipango mipya.

Akizungumza usiku wa kuamkia leo wakati wa Iftar iliyoandaliwa na wanawake wa Tume ya Madini Makao Makuu jijini Dodoma, Dkt. Lekashingo alisema mafanikio huanza kwa hatua ndogo ndogo zinazotekelezwa kwa nidhamu na uthabiti ndani ya muda mfupi.

Alieleza kuwa badala ya kusubiri kuanza kwa mwaka mpya ili kufanya mabadiliko, ni vyema kila mtu kujiuliza ni mambo gani anaweza kuyafanya ndani ya kipindi cha wiki 12 ili kuboresha afya yake, kuongeza ujuzi au kuleta mabadiliko chanya katika maisha yake.

Alisisitiza kuwa mabadiliko makubwa hayahitaji muda mrefu kama wengi wanavyodhani, bali yanahitaji kipindi kifupi chenye nidhamu, dhamira ya dhati na utekelezaji thabiti wa malengo yaliyowekwa.

“Endapo mtu ataweka malengo wazi na kuyasimamia kwa umakini, ndani ya muda mfupi anaweza kushuhudia mabadiliko makubwa katika maisha yake,” alisema.

Dkt. Lekashingo alibainisha kuwa mafanikio si suala la bahati, bali hutokana na nidhamu, juhudi binafsi na uwajibikaji, akisisitiza umuhimu wa kuwa na malengo yanayoeleweka na kuyatekeleza bila kukata tamaa.

Aidha, aliwataka wanawake kutoacha watu wengine waamue hatima ya maisha yao, akieleza kuwa mwanamke mwenye ujasiri na maono ana uwezo wa kubadilisha si tu maisha yake binafsi, bali pia maisha ya watu wengi na hata kizazi kizima.

Pia alisisitiza umuhimu wa kujenga urithi katika kazi, akiwahimiza watumishi kujiuliza ikiwa baada ya miaka 10 au 20 sekta ya madini itakapotajwa, kama wataweza kukumbukwa kwa mchango wao katika kuibadilisha na kuikuza.

Iftar hiyo ilihudhuriwa pia na Makamishna wa Tume ya Madini, Dkt. Theresia Numbi na Mhandisi Theonestina Mwasha, ambao waliwapongeza wanawake wa Tume kwa upendo, mshikamano na uchapakazi wao, huku wakiwahimiza kuendelea kumtanguliza Mungu katika kila jambo wanalofanya.







No comments:

Post a Comment