Wanawake wahimizwa kukuza malezi bora kwa wasichana - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 9, 2026

Wanawake wahimizwa kukuza malezi bora kwa wasichana



Na Mwandishi wetu,Kongwa


WANAWAKE wa Tawi la TUGHE Wizara ya Mifugo na Uvuvi wametumia Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kutoa wito kwa wanawake kujikita katika shughuli za kiuchumi na kuwalea wasichana katika misingi ya kujitegemea ili kuwa mama bora wa baadaye.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika wilayani Kongwa mkoani Dodoma, Katibu wa Tawi la TUGHE Wanawake Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Grace Mwaiselage, alisema wanawake wote waendelee kuwaelimisha wasichana kuhusu umuhimu wa kujishughulisha na shughuli za maendeleo tangu wakiwa na umri mdogo ili waweze kujitegemea na kuchangia ustawi wa familia na jamii kwa ujumla huku akisema hao ndiyo akina mama wajao.

Amewashukuru wanawake kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki siku hiyo muhimu inayotambua mchango wa wanawake katika jamii.

Mwaiselage pia ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Katibu Mkuu pamoja na Mradi wa Programu ya Uendelezaji Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe Maji katika Ukanda wa Pwani (TASFAM) kwa kusaidia kufanikisha maadhimisho hayo.

Amesema mradi huo unatoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wanawake ikiwemo miradi ya ufugaji wa samaki ambayo inaweza kuwasaidia wanawake kujipatia kipato na kuboresha maisha ya familia zao.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Tawi hilo, Joyce Mamkwe, amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inalenga kujumuisha wanawake katika mnyororo mzima wa thamani ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo.

Mamkwe amesema wanawake wanatarajia kunufaika na mradi wa TASFAM ambao una lengo la kuwawezesha kiuchumi na kuimarisha ushiriki wao katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Ameongeza kuwa wanawake wa tawi hilo wako tayari kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inaleta manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Naye Afisa kutoka Idara ya Uendelezaji wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Teddy Salema, aliishukuru wizara kwa kuwapa kibali cha kushiriki katika maadhimisho ya siku hiyo muhimu kwa wanawake.

Salema amezihimiza taasisi nyingine kuiga mfano wa mradi wa TASFAM kwa kuweka kipaumbele katika uwezeshaji wa wanawake kwani wakipewa nafasi wana uwezo mkubwa wa kuleta maendeleo katika jamii.

Amesema wanawake katika sekta ya mifugo wanafanya vizuri katika maeneo mbalimbali ikiwemo ufugaji, utoaji wa chanjo pamoja na uzalishaji wa malisho na vyakula vya mifugo.

“Wanawake wengi wanashiriki katika uzalishaji wa malisho na wako mstari wa mbele kuhakikisha mifugo inapata chakula bora, jambo linalosaidia upatikanaji wa nyama na maziwa bora pamoja na kuboresha afya ya mifugo na kuongeza pato la taifa,” amesema.

Amesisitiza kuwa wanawake wakipewa fursa na kuwezeshwa wanaweza kufanya mambo makubwa na kuleta maendeleo makubwa katika Taifa.

No comments:

Post a Comment