WAZIRI MKUU: COCO BEACH HAIUZWI, NI YA WANANCHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, March 29, 2026

WAZIRI MKUU: COCO BEACH HAIUZWI, NI YA WANANCHI


Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa ufafanuzi rasmi kuhusu hatma ya eneo la Coco Beach, akisisitiza kuwa halitauzwa kwa mwekezaji yeyote bali maboresho yatafanyika kwa manufaa ya wananchi waliopo katika eneo hilo.

Amesema hayo leo, Machi 29, 2026, alipotembelea eneo la Coco Beach jijini Dar es Salaam, ambapo alizungumza na wajasiriamali wadogo wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo na kusikiliza kero zao mbalimbali.

“Coco Beach haiuzwi. La kwanza niwaondolee hofu—hapauzwi, wala hakuna mwekezaji mwingine zaidi yenu nyinyi wenyewe. Hakuna atakayekuja kutoa maelekezo zaidi ya yale yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hapa hapauzwi,” amesisitiza.

Aidha, Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wananufaika na maboresho yanayofanyika katika eneo hilo.

“Sisi wasaidizi wa Mheshimiwa Rais tutaendelea kuhakikisha Watanzania wanapata lile tabasamu la Mama ambalo amewaahidi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amewataka watendaji wa Manispaa ya Kinondoni, akiwemo Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri, Afisa Biashara pamoja na watendaji wengine, kubadili mtindo wa utendaji kazi kwa kuwafuata wananchi moja kwa moja badala ya kuwasubiri ofisini.

“Ninatoa agizo kwa Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, Afisa Biashara pamoja na watendaji wengine—msikae ofisini tu. Tokeni mkazungumze na wananchi hawa moja kwa moja pale wanapokuwa na masuala yanayowahusu,” amesisitiza.

Kadhalika, Dkt. Mwigulu amewahimiza wajasiriamali wa eneo la Coco Beach kuunga mkono juhudi za Serikali katika maboresho yanayoendelea kufanyika, huku akisisitiza kuwa fursa zitakazotokana na maboresho hayo zitawanufaisha wao wenyewe.

No comments:

Post a Comment