DKT. STELLAH MPAGAMA ANG’ARA DUNIANI, AIPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA KATIKA SAYANSI NA AFYA AFRIKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, April 7, 2026

DKT. STELLAH MPAGAMA ANG’ARA DUNIANI, AIPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA KATIKA SAYANSI NA AFYA AFRIKA


Katika hatua inayoendelea kuipa heshima Tanzania kwenye ramani ya sayansi na afya duniani, Dkt. Stellah Mpagama ametajwa miongoni mwa viongozi wa afya duniani kutoka Afrika, akitambuliwa kwa mchango wake mkubwa katika utafiti wa kifua kikuu na magonjwa nyemelezi.

Dkt. Mpagama anaungana na majina makubwa barani Afrika yaliyolelewa na programu za European and Developing Countries Clinical Trials Partnership (EDCTP), ambazo kwa zaidi ya miongo miwili zimekuwa chachu ya mafanikio kwa wanasayansi wanaopambana na magonjwa ya kuambukiza katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kupitia programu hizo, Afrika imezalisha wataalamu waliobadilisha kabisa taswira ya mapambano dhidi ya magonjwa hatari. Miongoni mwao ni Abdoulaye Djimdé, bingwa wa tafiti za malaria na usugu wa dawa; Christian Happi, anayesifika kimataifa katika jenomiki, pamoja na Cissy Kityo, aliyekuwa mstari wa mbele katika mapinduzi ya tiba ya VVU nchini Uganda.

Wengine ni Delese Mimi Darko, kiongozi katika udhibiti wa dawa barani Afrika; Marieke van der Zalm, mtaalamu wa kifua kikuu kwa watoto na Nicaise Ndembi, anayejulikana kwa kuunganisha tafiti na sera za afya.

Orodha hiyo pia inawajumuisha Pauline Byakika, mtafiti wa malaria na mwingiliano wa dawa, Salim Abdool Karim, mtaalamu mashuhuri wa magonjwa ya mlipuko, pamoja na Tulio de Oliveira, kinara wa uchunguzi wa magonjwa kwa kutumia data za jenomu.

Kutajwa kwa Dkt. Mpagama katika orodha hiyo si tu heshima binafsi, bali pia ni ishara ya mchango mkubwa wa Tanzania katika mapambano ya kimataifa dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na uthibitisho kuwa Afrika ina sauti na nafasi muhimu katika mustakabali wa afya duniani.

No comments:

Post a Comment