POMBE NA VILAINISHI BANDIA VYAKAMATWA SINZA NA KARIAKOO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, April 7, 2026

POMBE NA VILAINISHI BANDIA VYAKAMATWA SINZA NA KARIAKOO

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WIZARA ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Tume ya Ushindani (FCC), imefanya operesheni maalum jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kukamata jumla ya bidhaa bandia 99,100 katika maeneo ya Sinza, Kariakoo na Pugu.

Operesheni hiyo iliyofanyika leo Aprili 7, 2026, ilibaini uwepo wa uzalishaji mkubwa wa pombe kali bandia pamoja na vilainishi feki vya mafuta, hali inayotajwa kuwa tishio kwa afya ya wananchi na uchumi wa Taifa.

Katika msako huo, mamlaka zilifanikiwa kunasa kiwanda kinachozalisha pombe kali bandia aina ya Konyagi katika eneo la Sinza A, wilayani Kinondoni, ambapo chupa 4,000 zenye ujazo wa mililita 200 pamoja na katoni 250 tupu zenye nembo ya bidhaa hiyo zilikamatwa.

Aidha, pombe nyingine bandia aina ya Valuer Gin na Smartgin zilikamatwa katika eneo la Pugu, wilayani Ilala, zikiongeza ushahidi wa kuenea kwa mtandao wa uzalishaji wa bidhaa zisizo halali.

Kwa upande wa vilainishi vya mafuta, zaidi ya chupa 5,000 zilikamatwa katika eneo la Kariakoo, zikiwa zimefungashwa kwa kutumia mafuta machafu katika vifungashio vya chapa maarufu, hatua inayohatarisha watumiaji pamoja na kuathiri ubora wa mitambo na vyombo vya moto.

Akizungumza kuhusu operesheni hiyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Judith Kapinga, alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kudhibiti bidhaa bandia zinazoathiri afya ya wananchi na kupunguza mapato ya Serikali.

Amesema mbali na bidhaa hizo kukamatwa, pia jumla ya bidhaa 11,000 kutoka kampuni nne zimeondolewa sokoni na kushikiliwa zikisubiri kukamilika kwa taratibu za kisheria.

“Bidhaa hizi zina madhara makubwa kwa afya ya jamii na husababisha uharibifu wa haraka wa mitambo na vyombo vya moto, hali inayosababisha hasara kwa watumiaji na Taifa kwa ujumla,” amesema Kapinga.

Ametoa wito kwa wananchi kuwa makini wanaponunua bidhaa kwa kuhakiki alama za ubora kupitia mfumo wa ‘Hakiki’ wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), huku akiwataka wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa uadilifu na kurasimisha biashara kupitia taasisi kama TBS na BRELA.

Kapinga amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa bandia ili kulinda wawekezaji halali na kuhakikisha ushindani wa haki sokoni.

Ameongeza kuwa operesheni hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha uchumi wa nchi kwa kudhibiti biashara haramu zinazohatarisha afya za wananchi na kupunguza mapato ya Taifa.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 7, 2026 Jijini Dar es Salaam mara baada ya kuendesha operesheni ya ukaguzi wa bidhaa bandia viwandani.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO

No comments:

Post a Comment