Na Shua Ndereka OKULY BLOG, Morogoro
Mfumo wa stakabadhi ghalani umeendelea kuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima, ukionyesha wazi kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa taifa katika msimu wa mwaka 2025/2026.
Mfumo huo umeingiza mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 90 kwa Mkoa wa Morogoro, hatua inayodhihirisha kuwa juhudi zikitiwa nguvu, matunda yake huwa ya kuridhisha.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mfumo huo mwishoni mwa Machi 2026, ambapo amesema mapato hayo yameongezeka kutoka shilingi bilioni 71 katika msimu uliopita hadi kufikia zaidi ya bilioni 90.
Malima amesisitiza kuwa Mkoa umejipanga kuongeza uzalishaji zaidi ili kufikia mafanikio makubwa.
Naye Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro, Cesilia Sostenes, ameeleza namna mfumo huo ulivyoimarisha ushirika na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima, hali inayowawezesha kunufaika zaidi na jasho lao pamoja na kukuza uchumi wa Morogoro kwa ujumla.
“Kwa msimu 2025/2026 Mkoa wa Morogoro ulifanya minada 128 kwa mazao ya mbaazi, ufuta, korosho na kakao, ambapo jumla ya kilo 151,522,755 zenye thamani ya 98,275,357,791.42, huku wakulima wakilipwa jumla ya shilingi 88,897,268,932.35 katika fedha hizo,” amesema Cesilia.
Aidha, Cesilia ameeleza kuwa, kwa msimu uliopita, mazao hayo yamechangia katika halmashauri zao kiasi cha shilingi 2,902,250,972.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Denis Londo, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wakulima na wafanyabiashara huku ikihamasisha uwepo wa viwanda vyenye ushindani, akibainisha kuwa maendeleo hayaji kwa bahati bali kwa mipango thabiti.
“Uwekezaji mkubwa kwenye ushirika unampa nguvu mkulima, unamuongezea tija ya mazao yake ambapo atapata pato linalofanana na jasho aliloweka,” amesema Londo.
Hata hivyo, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, amesisitiza usimamizi bora wa vyama vya ushirika ili kuendeleza mfumo huo kwa tija na kuleta mabadiliko chanya kwa wakulima na uchumi wa taifa kwa ujumla.







No comments:
Post a Comment