Wachimbaji wadogo wa madini ya ujenzi katika Mkoa wa Tanga wamepata fursa ya kupatiwa mafunzo maalum ya kitaalamu yanayotolewa na Tume ya Madini Tanzania kwa kushirikiana na UNDP pamoja na Foundation for ASM Development, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha sekta ya uchimbaji mdogo nchini.
Mafunzo hayo, yanayofadhiliwa na UNDP, yanalenga kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi, usalama, na tija kubwa kiuchumi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mratibu wa Miradi kutoka FADev, Bi. Rehema Mkuli, alieleza kuwa lengo kuu ni kuwainua wachimbaji wanaojihusisha na madini ya ujenzi na viwanda, hususan limestone, kwa kuwapatia maarifa ya kitaalamu yatakayosaidia kuboresha uzalishaji na kulinda mazingira.
Aliongeza kuwa washiriki wanapatiwa mafunzo muhimu ikiwemo mbinu za msingi za uchoraji wa ramani za kijiolojia (Basic Geological Mapping) pamoja na usanifu salama na bora wa mashimo ya uchimbaji (Safe and Efficient Pit Design), ambayo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha uchimbaji unafanyika kwa usahihi na kwa kuzingatia usalama.
Kwa upande wake, Mkufunzi kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tanga, Mjiolojia Daudi, aliwahimiza wachimbaji kuongeza juhudi katika kujifunza utambuzi wa aina mbalimbali za miamba na kuelewa madini yaliyomo ndani yake.
Alisisitiza kuwa uelewa huo utasaidia kupunguza uchimbaji wa kubahatisha na kuongeza ufanisi katika utambuzi wa rasilimali.
Mafunzo haya yanatajwa kuwa hatua muhimu katika kukuza uchimbaji mdogo wenye tija, kuongeza kipato kwa wachimbaji, na kuchangia maendeleo endelevu ya sekta ya madini nchini Tanzania.






No comments:
Post a Comment