ZAIDI YA BILIONI 517 KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA DAR ES SALAAM KUPITIA DMDP II - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, April 1, 2026

ZAIDI YA BILIONI 517 KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA DAR ES SALAAM KUPITIA DMDP II



‎Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam

‎Zaid ya Bilioni 517 zimeelekezwa kuboresha miundombinu ya barabara Mkoa wa Dar es Salaam kupitia Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II) hatua inayolenga kuondoa changamoto ya usafiri na kukuza ukuaji wa uchumi.

Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga ameeleza kuwa mradi huo umekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto ya miundombinu ya barabara mkoani humo.
‎Amesema kuwa serikali kupitia TARURA inaendelea na maboresho na matengenezo ya barabara zenye urefu wa Km 250 kwa kiwango cha lami katika wilaya zote tano (5) za mkoa wa Dar es Salaam ambazo zinagharimu shilingi Bilioni 516 ili kuchochea shughuli za kiuchumi na biashara ndani ya mkoa.

‎"TARURA mkoa wa Dar es Salaam tuna mtandao wa barabara Km 5057 kati ya hizo lami ni Km 677 sawa na asilimia 13 huku barabara za udongo zipo zaidi ya Km 2500 sawa na asilimia 50 ya mtandao wote, ujenzi wa barabara za lami zitapunguza barabara za udongo ili kuboresha huduma za usafiri na usafishaji, kupunguza foleni na changamoto za mafuriko, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi", alisema.

‎Aliongeza kuwa pamoja na changamoto ya mvua lakini kazi zinaendelea vizuri ili zikamilike kwa wakati ambapo utekelezaji umefikia zaidi ya asilimia 80 huku wanatarajia barabara nyingi zitakamilika na kuanza kutumika mwezi Agosti hadi Oktoba 2026 mpaka mwezi Aprili 2027.

‎"Barabara ya Banana hadi Kivule, barabara ya Mbezi Msumi zilikuwa na kilio kikubwa kutoka kwa wananchi mpaka ifikapo mwezi 8 mpaka wa 10 barabara hizi zitakamilika, katikati ya mji Kariakoo ambapo ni eneo la kibiashara barabara nyingi zilikuwa hazipitiki zina matope, maboresho yanaendelea na maeneo mengine mengi ndani ya mkoa wetu maboresho yanaendelea", alisema.

‎Amewaomba wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho ujenzi unaendelea na miundombinu hiyo itakapokamilka wananchi wawe walinzi na watunzaji wa miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

‎Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa mkoa huo wameishukuru serikali kwa kuboreshewa miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali ambapo wamesema miundombinu hiyo ikikamilika itaboresha shughuli za usafiri na usafirishaji na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii.



No comments:

Post a Comment