
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeishauri Serikali kuandaa mkakati wa kuviwezesha Vyuo Vikuu vyote vinavyotoa kozi za afya nchini kuwa na hospitali za mafunzo kwa vitendo (teaching hospitals) ili kuongeza ufanisi wa mafunzo kwa wanafunzi wa kada za afya.
Maoni hayo yamewasilishwa bungeni na Asha Juma Ferouz kwa niaba ya Kamati hiyo wakati akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na maoni, ushauri na mapendekezo ya Kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Asha amesema Kamati imebaini kuwa baadhi ya Vyuo Vikuu vinavyotoa kozi za afya havina hospitali za mafunzo kwa vitendo hali inayosababisha wanafunzi kukosa uzoefu wa moja kwa moja katika mazingira halisi ya utoaji huduma za afya.
Amesema changamoto hiyo inaathiri ubora wa elimu ya tiba pamoja na huduma za afya kwa ujumla kutokana na wanafunzi kutopata mafunzo ya kutosha kwa vitendo.
Kutokana na hali hiyo, Kamati imependekeza Serikali kuandaa mkakati maalum wa kuhakikisha vyuo vyote vinavyotoa kozi za afya vinakuwa na hospitali za mafunzo kwa vitendo ili kuwajengea wanafunzi uwezo na ujuzi unaohitajika kabla ya kuhitimu masomo yao.
Kamati hiyo imetoa mfano wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ikieleza kuwa kinaweza kutumia Hospitali ya Mloganzila kama hospitali ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wake.
Mbali na hilo, Kamati imeishauri Serikali kuhakikisha fedha za miradi ya elimu zinatolewa kwa wakati ili kuharakisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika sekta hiyo.
Aidha, Kamati imeitaka Serikali kutoa fedha za Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kwa ukamilifu kwa wanafunzi wote wenye sifa za kupata mikopo hiyo ili kupunguza changamoto za kifedha kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Katika taarifa hiyo, Kamati pia imependekeza kuongezwa kwa fedha za uchapaji wa vitabu ili kuboresha uwiano wa kitabu na mwanafunzi pamoja na kuongeza bajeti ya mafunzo kazini kwa walimu wa lugha ya alama ili kuimarisha elimu jumuishi nchini.








No comments:
Post a Comment