Serikali imesema itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB) ili kuhakikisha sekta ya uhandisi na teknolojia inaendelea kuchangia kikamilifu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050.
Hayo yamesemwa leo Mei 7, 2026 Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, aliyemwakilisha Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 8 wa Mafundi Sanifu Tanzania wa mwaka 2026.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Msando amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa mafundi sanifu na wataalamu wa uhandisi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo ujenzi wa Miundombinu ya barabara, madaraja, majengo, reli na miundombinu mingine muhimu.
Amesema ili kufikia malengo ya maendeleo ya teknolojia na uchumi wa kisasa, kuna umuhimu mkubwa kwa Bodi ya usajili wa Wahandisi ERB kuendeleza mchakato wa usajili wa mafundi sanifu wenye sifa na weledi watakaoongeza nguvu kazi ya kitaalamu inayohitajika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ufanisi na viwango vinavyokubalika.
“Serikali itaendelea kushirikiana na ERB katika kuhakikisha taaluma ya uhandisi inaimarika zaidi na wataalamu wanaendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, ubunifu pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa,” amesema Msando.
Aidha, amewataka wahandisi na mafundi sanifu wapya waliokula kiapo katika mkutano huo kuzingatia maadili ya taaluma yao na kusimamia miradi kwa uadilifu, uwajibikaji na weledi mkubwa ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inaleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi ya usajili wa Wahandisi ERB, Profesa, Bakari Mwinyiwiwa ameeleza kuwa bodi hiyo itaendelea kuweka mazingira bora ya kukuza taaluma ya uhandisi nchini pamoja na kuimarisha usimamizi wa wataalamu ili kuhakikisha huduma za uhandisi zinakuwa salama, bora na zenye kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani.
Mkutano huo wa siku mbili unahusisha mafundi sanifu, wahandisi, wadau wa sekta ya ujenzi pamoja na wanafunzi wa taaluma za uhandisi kutoka taasisi mbalimbali za elimu huku ikilengwa kujadili nafasi ya teknolojia, ubunifu na utaalamu katika kuharakisha maendeleo ya Tanzania kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.










No comments:
Post a Comment