MHE. SALOME: NYUMBA 2,512 ZIMEUNGANISHWA NA MIUNDOMBINU YA GESI ASILIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 8, 2026

MHE. SALOME: NYUMBA 2,512 ZIMEUNGANISHWA NA MIUNDOMBINU YA GESI ASILIA


Na Mwandishi Wetu


Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amesema hadi Aprili 2026, jumla ya nyumba 2,512 zimeunganishwa na miundombinu ya gesi asilia katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam.

Mhe. Salome ametoa taarifa hiyo Mei 8, 2026 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Asha Omar Rashid, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuboresha upatikanaji wa nishati ya gesi vijijini.

Akijibu swali hilo, Mhe.Salome amesema Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya usambazaji wa gesi asilia, ambapo hadi Aprili 2026 nyumba 425 zimeunganishwa katika Mkoa wa Mtwara, 677 Mkoa wa Lindi, 530 Mkoa wa Pwani na 880 Mkoa wa Dar es Salaam.

Aidha, amesema katika kuhakikisha nishati ya gesi inawafikia Watanzania wengi zaidi, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea kutekeleza mradi wa kusambaza mitungi 452,445 ya Gesi Oevu ya Petroli (LPG) yenye ujazo wa kilogramu sita kwa ruzuku ya asilimia 50 ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika maeneo ya vijijini na vijiji-miji.

Vilevile, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika miundombinu ya usambazaji wa gesi ya LPG katika maeneo ya vijijini na vijiji-miji.

Mhe. Salome amesema Serikali pia inaendelea kufanya tafiti katika maeneo ya mijini na vijijini ili kubaini aina sahihi ya miundombinu inayohitajika kwa ajili ya kufikisha na kusambaza gesi asilia kwa ufanisi zaidi.

Amefafanua kuwa matokeo ya tafiti hizo yatawezesha kubainisha njia bora za usambazaji wa gesi asilia kulingana na mahitaji ya maeneo husika, sambamba na kuibua fursa za kuanzishwa kwa miradi mingine ya usambazaji wa gesi asilia itakayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi mijini na vijijini wananufaika na nishati hiyo safi.

No comments:

Post a Comment