WANANCHI WA KALENGA WAUNGANA KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINISIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 8, 2026

WANANCHI WA KALENGA WAUNGANA KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINISIA



Na Herieth Molla, Iringa


Juhudi za kupambana na ukatili wa kijinsia zinaendelea kushika kasi katika Kata ya Kalenga, Wilaya ya Iringa, huku wananchi wakiungana kwa karibu na serikali pamoja na vyombo vya usalama ili kukomesha vitendo hivyo.

Wananchi wa eneo hilo wanasema sasa kila mmoja ameanza kutambua na kutekeleza wajibu wake katika kupinga ukatili wa kijinsia kwa vitendo.

Juhudi hizo zimepata nguvu zaidi kufuatia kuanzishwa kwa Kituo cha Taarifa na Maarifa (KC) kinachosimamiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), ambacho kimekuwa kikitoa elimu na uhamasishaji kwa jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia na umuhimu wa kutoa taarifa kwa wakati.

Kwa mujibu wa wananchi wa Kalenga, elimu wanayoipata kupitia kituo hicho imeongeza uelewa wao kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia, kusaidia kufichua matukio yaliyokuwa yakifichwa, pamoja na kuwajengea uwezo wa kuripoti matukio hayo kwa wakati. Wanasema hatua hiyo imeanza kuleta mabadiliko chanya ndani ya jamii, huku watu wengi wakitambua wajibu wao katika kupinga vitendo hivyo.

Mzee wa kimila katika kata hiyo, Zuberi Witala, amesema elimu hiyo imewasaidia wanaume wengi kutambua baadhi ya vitendo walivyokuwa wakivifanya kwa mazoea bila kufahamu kuwa ni ukatili dhidi ya wenza wao.

“Kupitia elimu hii tumesaidika sana. Imetufanya tuachane na baadhi ya mila kandamizi ambazo zilikuwa zimezoeleka katika jamii yetu. Sasa tunaendelea kuwaelimisha wengine,” amesema Mzee Witala.

Naye mkazi wa Kalenga, Khalid Ismail, amesema elimu hiyo imechangia kurejesha amani ndani ya familia nyingi na kusaidia wazazi kuwafundisha watoto kushirikiana katika kazi za nyumbani bila ubaguzi wa kijinsia.

“Elimu hii imetusaidia hata katika mgawanyo wa majukumu ya kifamilia tofauti na zamani. Hali hiyo imeleta furaha na amani ndani ya familia zetu,” amesema Khalid.

Kwa upande wake, Polisi Kata wa Kalenga, Koplo Editha Kayuni, amepongeza juhudi za Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kuendelea kutoa elimu katika eneo hilo. Amesema hatua hiyo imeimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi na kusaidia upatikanaji wa taarifa za matukio ya ukatili kwa haraka zaidi.

“Tunalishukuru shirika la TGNP kwa elimu hii kwani imetusaidia kuwa karibu zaidi na wananchi na kupata taarifa za matukio kwa wakati. Sisi wenyewe hatuwezi kugundua matukio yote bila ushirikiano kutoka kwa wananchi,” amesema Koplo Kayuni.

Hata hivyo, wananchi wameeleza changamoto wanazokumbana nazo katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, ikiwemo baadhi ya watuhumiwa kupewa dhamana, jambo ambalo wanasema linaweza kuathiri ushahidi na kuongeza hofu kwa wahanga.

Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kalenga, Peter Mvula, amesema kuna haja ya kuimarishwa kwa sheria ili kudhibiti vitendo hivyo.

“Nafikiri sheria zinapaswa kuwekewa mkazo zaidi, hasa kwa wanaotuhumiwa kwa makosa kama ubakaji na ulawiti. Endapo watuhumiwa hawatapewa dhamana hadi kesi zao zitakapomalizika, inaweza kusaidia kupunguza matukio haya,” amesema Mvula.

Akijibu hoja hiyo, Koplo Kayuni amesema Jeshi la Polisi lina wajibu wa kusimamia sheria zilizopo, ikiwemo haki ya dhamana kwa mujibu wa sheria za nchi.

Aidha, amewahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kufuatilia kesi wanazoripoti na kutoa ushirikiano mahakamani ili kuhakikisha wahanga wanapata haki zao na watuhumiwa wanachukuliwa hatua stahiki.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Iringa, Gladness Amulike, amesema halmashauri inaendelea kushirikiana na wananchi katika kuwasaidia wahanga wa ukatili wa kijinsia kupata msaada wa kisheria pamoja na huduma za nyumba salama kwa ajili ya kulinda usalama wao.


Kwa upande wake, Mshauri wa Afya ya Uzazi na Masuala ya Jinsia, Dkt. Katanta Lazarus Simwanza, amesema licha ya changamoto zilizopo, jamii ina uwezo mkubwa wa kushinda vita dhidi ya ukatili wa kijinsia iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake ipasavyo.

No comments:

Post a Comment