SERIKALI KUBORESHA UALIMU KWA KUIMARISHA MAENDELEO YA WALIMU NA MAFUNZO YA VITENDO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 7, 2026

SERIKALI KUBORESHA UALIMU KWA KUIMARISHA MAENDELEO YA WALIMU NA MAFUNZO YA VITENDO



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na maendeleo ya taaluma ya ualimu nchini kupitia utekelezaji wa majukumu ya Bodi ya Kitaalamu ya Walimu Tanzania (Tanzania Teachers Professional Board), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda na kuinua hadhi ya taaluma hiyo.

Kupitia hatua hiyo, Serikali itaandaa mwongozo wa viwango vya ufundishaji ili kukuza mafunzo endelevu kwa walimu, pamoja na kuandaa Mwongozo wa Maadili na Mwenendo wa Taaluma ya Ualimu utakaosaidia kuimarisha nidhamu na weledi katika sekta ya elimu.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Katika hatua nyingine, Serikali itaanza kutekeleza mpango wa mafunzo kwa vitendo wa mwaka mmoja (internship) kwa wahitimu wa mafunzo ya ualimu, hatua inayolenga kuwawezesha walimu tarajali kuoanisha maarifa ya nadharia na uhalisia wa kazi darasani.

Aidha, Serikali itaendelea kuwajengea uwezo walimu wa shule za msingi na sekondari, wakufunzi wa vyuo vya ualimu, wathibiti ubora wa shule na wasimamizi wa elimu ili kuboresha utendaji katika sekta ya elimu.

Katika mpango huo, walimu 1,223 watanufaika na ufadhili wa masomo ya Stashahada ya Ualimu wa Elimu Maalum, huku walimu 3,000 wakipatiwa mafunzo ya ushauri na unasihi kuhusu malezi, stadi za maisha na ulinzi wa mtoto.

Vilevile, watendaji 5,500 pamoja na walimu na wanafunzi watanufaika na mafunzo kuhusu matumizi ya majukwaa ya kielimu, ikiwemo maktaba mtandao na majukwaa ya kujifunza mtandaoni kwa lengo la kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika elimu.

No comments:

Post a Comment