
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Serikali kupitia taasisi za elimu ya juu na elimu ya ufundi inatarajia kutekeleza miradi 1,390 ya utafiti katika mwaka wa fedha 2026/27, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha sayansi, teknolojia na ubunifu kwa lengo la kuchochea uchumi wa viwanda nchini.
Aidha, Serikali itaongeza ufadhili wa miradi ya utafiti na ubunifu kutoka 80 hadi 109, hatua inayolenga kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uchumi wa bluu, uvuvi, maji, kilimo, afya na viwanda.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Katika kuimarisha usambazaji wa maarifa, Serikali pia inatarajia kuchapisha machapisho 2,497 katika majarida ya kitaifa na kimataifa ili kukuza mijadala ya kitaaluma na kuhakikisha matokeo ya utafiti yanatumika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
Vilevile, Serikali itaimarisha uwezo wa maabara katika taasisi tano za utafiti na maendeleo ili ziwe maabara za rufaa za utafiti na ubunifu wa viwanda, sambamba na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za utafiti, vyuo vya elimu ya juu na sekta ya viwanda.
Kwa upande wa ubunifu, Serikali itaendelea kuhamasisha wabunifu kupitia mfuko wa Samia Innovation Commercialization Fund, pamoja na kubadilisha vyuo vitano vya maendeleo ya wananchi kuwa vituo vya ubunifu.
Katika sekta ya teknolojia ya nyuklia, Serikali pia itakagua vituo 900 vyenye vyanzo vya mionzi na kudhibiti viwango vya mionzi kwa wafanyakazi 2,110 ili kulinda afya za wananchi, wafanyakazi na mazingira kwa ujumla.

No comments:
Post a Comment