WANAFUNZI 292,981 KUNUFAIKA NA MIKOPO 2026/27 - PROF. MKENDA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 7, 2026

WANAFUNZI 292,981 KUNUFAIKA NA MIKOPO 2026/27 - PROF. MKENDA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Wanafunzi 292,981 wanatarajiwa kunufaika na mikopo ya elimu ya juu katika mwaka wa fedha 2026/27, ikiwa ni ongezeko kutoka 252,773 wa mwaka 2025/26, katika hatua inayolenga kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu nchini.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Katika mpango huo, Serikali pia imetangaza kuratibu udahili wa wanafunzi 180,000 watakaojiunga na programu mbalimbali za shahada ya kwanza katika vyuo vya elimu ya juu nchini.

Aidha, wanafunzi 24,978 wa stashahada katika fani za sayansi na ufundi wataendelea kunufaika na mikopo hiyo, kama sehemu ya kuimarisha elimu ya ufundi na taaluma za sayansi.

Kwa upande wa masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM), idadi ya wanufaika wa SAMIA Scholarship imeongezwa kutoka 2,630 hadi 2,738, huku programu ya Samia Extended Scholarship DS/AI+ ikiongeza nafasi za wanafunzi kusoma nje ya nchi kutoka 50 hadi 100 katika fani za sayansi data, sayansi shirikishi na akili unde (AI).

Serikali pia itaendelea kutoa ufadhili katika eneo la sayansi na teknolojia ya nyuklia kwa wanafunzi wa shahada ya umahiri, ikiwa ni mkakati wa kuandaa wataalamu wa teknolojia za kisasa nchini.

No comments:

Post a Comment