SERIKALI YASAJILI SHULE 671, YASAMBAZA ZAIDI YA VITABU MILIONI 11 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 7, 2026

SERIKALI YASAJILI SHULE 671, YASAMBAZA ZAIDI YA VITABU MILIONI 11



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Serikali imeendelea kuongeza fursa za elimu nchini kwa kusajili shule 671 zikiwemo shule 23 za awali, shule 401 za awali na msingi, shule 245 za sekondari pamoja na vyuo viwili vya ualimu katika jitihada za kuboresha upatikanaji wa elimu kwa watoto na vijana nchini.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Prof. Mkenda amesema Serikali imeendelea kuwezesha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya elimu ikiwemo mabweni sita katika shule za sekondari, madarasa 128, bwalo la chakula, nyumba ya mwalimu pamoja na ukarabati wa shule mbili za sekondari ili kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.

Aidha, amesema Serikali imeimarisha uthibiti ubora wa elimu kwa kufanya tathmini ya jumla katika asasi 8,067 zikiwemo shule za awali, msingi, sekondari, vyuo vya ualimu, vituo vya elimu nje ya mfumo rasmi pamoja na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.

Ameeleza kuwa asasi zilizobainika kuwa na changamoto mbalimbali zilipewa ushauri wa kitaalamu ili kuboresha utoaji wa elimu.

Katika kuhakikisha upatikanaji wa vitabu vya kiada unaimarika, Waziri huyo amesema Serikali imechapa na kusambaza nakala 4,845,490 za vitabu vya darasa la tano pamoja na nakala 6,887,325 za vitabu na viongozi vya walimu kwa wanafunzi wa kidato cha pili.

Kwa mujibu wa Prof. Mkenda, kwa masomo ya sanaa uwiano wa vitabu ni kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu huku masomo ya sayansi yakifikia uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja.

Vilevile, Serikali imechapa na kusambaza nakala 3,000 za vitabu vya darasa la tano na nakala 31,520 za vitabu vya kidato cha pili kwa wanafunzi wenye uoni hafifu kwa uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja.

Kwa upande wa wanafunzi wasioona, amesema Serikali imechapisha na kusambaza nakala 9,600 za vitabu vya maandishi ya Breili kwa darasa la tano pamoja na nakala 8,362 za vitabu vya Breili kwa wanafunzi wa kidato cha pili ili kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata haki sawa ya elimu.

No comments:

Post a Comment