SHULE 10 ZAPATA MAABARA ZA TEHAMA, UDAHILI VYUO VYA UFUNDI WAFIKIA ASILIMIA 119 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 7, 2026

SHULE 10 ZAPATA MAABARA ZA TEHAMA, UDAHILI VYUO VYA UFUNDI WAFIKIA ASILIMIA 119



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania imewezesha ujenzi wa maabara za TEHAMA katika shule 10 za sekondari pamoja na kusambaza vifaa vya TEHAMA ikiwemo kompyuta za mezani 213 na kompyuta mpakato 24 kwa lengo la kuimarisha ubora wa ujifunzaji na matumizi ya teknolojia mashuleni.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Prof. Mkenda amesema uwekezaji huo unalenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa kutumia teknolojia katika maisha ya kila siku pamoja na kuwaandaa kwa ushindani katika soko la ajira.

Aidha, amesema Serikali imeendelea kuimarisha elimu jumuishi kwa kuandaa miongozo minane ya utoaji wa elimu hiyo ikiwemo Mwongozo wa Sanaa na Michezo Rekebifu kwa Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalum wa mwaka 2026, Mwongozo wa Matumizi ya TEHAMA na Teknolojia Saidizi pamoja na Mwongozo wa Lugha ya Alama ya Tanzania wa mwaka 2026.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Serikali imeandaa Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na wanafunzi wa darasa la kwanza na pili, uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Januari 29, 2026 jijini Dar es Salaam.

Amesema mpango huo unalenga kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayefika darasa la tatu bila kuwa na uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu.

Vilevile, amesema Serikali imeanzisha mpango wa pamoja kati ya waajiri, vyuo vya ufundi stadi na vyuo vikuu ili kuimarisha ujuzi wa wahitimu kulingana na mahitaji ya soko la ajira. Mpango huo ulizinduliwa Februari 9, 2026 na Makamu wa Rais, Emmanuel John Nchimbi jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, Prof. Mkenda amesema Serikali imedahili wanafunzi 315,307 ambapo wanafunzi 236,199 wamejiunga na vyuo vya elimu ya ufundi huku 79,108 wakijiunga na vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi, sawa na asilimia 119 ya lengo la kudahili wanafunzi 265,000.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na kuongezeka kwa idadi ya vyuo kutoka 1,414 mwaka 2025 hadi 1,446 mwaka 2026, hatua inayolenga kuongeza fursa za elimu ya ufundi na kujenga nguvu kazi yenye ujuzi nchini.

No comments:

Post a Comment