
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Zaidi ya wanafunzi 3,021,177 wanatarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari kidato cha kwanza ifikapo Januari 2028, kufuatia utekelezaji wa sera ya elimu ya lazima ya miaka 10 inayotekelezwa na Serikali kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Prof. Mkenda amesema idadi hiyo ya wanafunzi inatokana na wanafunzi waliopo darasa la tano na la sita mwaka 2026 ambao wanatarajiwa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2027 na kuanza sekondari mwaka 2028.
Amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeendelea na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo madarasa, maabara, karakana pamoja na ununuzi wa vifaa na kuajiri walimu wapya ili kuhakikisha wanafunzi hao wanapokelewa kwa wakati.
Aidha, amesema utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10 ni hatua ya kihistoria itakayoongeza upatikanaji wa elimu ya sekondari na kusaidia kuandaa vijana wenye ujuzi na maarifa yanayokidhi mahitaji ya maendeleo ya taifa na ajira.
Amefafanua kuwa chini ya mfumo mpya wa elimu, mtoto atamaliza elimu ya lazima akiwa na umri wa miaka 16 tofauti na mfumo wa awali ambapo mwanafunzi alimaliza darasa la saba akiwa na miaka 13, umri ambao hauwezi kumwezesha kuajiriwa au kujiajiri.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali pia imeendelea na maandalizi ya kuanzisha mkondo wa amali katika shule za sekondari ili kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kujitegemea na kukabiliana na changamoto za ajira.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali inaendelea na mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 ambapo tayari maoni ya wadau mbalimbali yamekusanywa na taarifa ya awali ya mapitio hayo imeandaliwa.
Sambamba na hilo, Serikali imeandaa viunzi mbalimbali vya kuimarisha sekta ya elimu ikiwemo Kiunzi cha Umahiri wa Walimu katika TEHAMA 2026 pamoja na Kiunzi cha Kitaifa cha Ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa teknolojia za kidijitali katika sekta ya elimu.

No comments:
Post a Comment