WAANDISHI WA HABARI WAPIGWA MSASA UTAYARISHAJI VIPINDI VYA WATOTO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 8, 2026

WAANDISHI WA HABARI WAPIGWA MSASA UTAYARISHAJI VIPINDI VYA WATOTO


Na WMJJWM – Dar es Salaam


Waandaaji wa vipindi vya watoto wamehimizwa
kutumia taaluma zao na lugha rafiki kwa watoto na vijana pamoja na
kuzingatia maadili ya taaluma ya Habari katika kuandaa maudhui yenye
ubora yatakayochangia ukuaji na maendeleo ya mtoto katika jamii.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa Programu ya malezi na familia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Victor RugalabamuMei 8, 2026
wakati wa kuhitimisha mafunzo maalum yaliyoandaliwa na Wizara hiyo kwa
kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia
watoto (UNICEF) kwa lengo la kuwajengea uwezo waandaaji wa vipindi wa radio za
jamii, Televisheni na Mitandao ya Kijamii katika kutengeneza maudhui
yanayofundisha, kuburudisha na kuhamasisha maadili mema kwa watoto.

Victor amesema,  kupitia mafunzo hayo, Wizara inatarajia kuona vipindi vitakavyorushwa kupitia vyombo vya habari  vinatoa mafunzo ya
maadili mema kwa kizazi cha sasa na kijacho pia vinahamasisha
malezi mazuri ndani ya familia na kuwasaidia watoto na vijana
balehe kukua katika mazingira salama, yenye upendo na ulinzi.

Kwa upande wake Mwezeshaji wa mafunzo hayo,
Sabrina Majikata kutoka Shirikia Lisilo la Kiserikali la ICS  amesema
mafunzo yamejikita kuwawezesha Waandishi wa Habari katika kutayarisha
vipindi bora  na kuzungumza kwa ufasaha katika  nguzo tatu ambazo ni
namna ya mzazi kumjali,  kumtunza na
kuzungumza na mtoto ili aweze kubaini changamoto zinazoweza kuathiri
maendeleo yake.

“Mwandishi wa habari anapokuwa na uelewa kuhusu ukuaji wa watoto
na changamoto zinazowakabili pamoja na vijana balehe, anakuwa
na uwezo mkubwa wa kutengeneza maudhui yenye manufaa kwa jamii. 
Kupitia mafunzo haya, tumesisitiza umuhimu wa kuandaa vipindi
vinavyolinda maslahi ya mtoto, vinavyotoa elimu sahihi na vinavyochochea mawasiliano mazuri ndani ya familia”. Amesema Sabrina

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia
Watoto (UNICEF) Alice Mwiru ambaye
ni Mtaalamu wa mabadiliko ya tabia za jamii, amehimiza waandishi wa habari kuongeza ubunifu na uwajibikaji katika utayarishaji wa vipindi vya Watoto, amesisitiza kuwa UNICEF itaendelea kushirikiana na
Serikali kuboresha maudhui yanayohusu watoto ili kuhakikisha haki za mtoto na masuala yao yanapewa kipaumbele katika majukwaa ya habari.

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Godliver Thomasi kutoka Jamii Forums amesema mafunzo hayo yamempa mwanga zaidi namna ya kuandaa vipindi husika.

“Mafunzo haya yamenipa uelewa mpana kuhusu namna ya kuandaa maudhui
yanayowagusa watoto na vijana kwa njia sahihi na yenye kujenga. Nimejifunza umuhimu wa kutumia lugha rafiki, kuzingatia hatua za
ukuaji wa mtoto pamoja na kuandaa vipindi vinavyofundisha na kuburudisha kwa wakati mmoja. Kupitia elimu hii, ninaamini nitakuwa sehemu ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii kupitia kazi yangu ya uandishi wa habari”

No comments:

Post a Comment