WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya barabara nchini na kuhakikisha sekta hiyo inakuwa kipaumbele kwa kuwa ndiyo msingi wa kufungua uchumi, kurahisisha usafirishaji wa mazao na kuchochea maendeleo ya wananchi vijijini na mijini.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo, Mei 24, 2026 alipokagua mradi wa ujenzi wa Barabara ya Iringa (Ipogolo) – Kilolo yenye urefu wa kilomita 33.61 kwa kiwango cha lami chini ya Programu ya RISE (Barabara kwa Maendeleo na Fursa za Kiuchumi na Kijamii) katika Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya miundombinu kwa lengo la kuimarisha shughuli za kiuchumi na kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi.
Amebainisha kuwa Serikali imekubaliana kuhakikisha miradi yote iliyoanza inakamilishwa kwanza, sambamba na kuendelea kutoa fedha za utekelezaji kwa miradi iliyosainiwa mikataba lakini haikupata malipo ya awali.
“Tunahakikisha kwanza tunakamilisha miradi ambayo ilikuwa imeanza, iliyosainiwa lakini haikupata malipo ya awali, pamoja na ile ambayo wakandarasi walishapatikana, ili wananchi waanze kunufaika na miradi hiyo,” amesema.
Aidha, amesema Serikali imeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mingine baada ya kukamilika kwa baadhi ya miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Bwawa la Julius Nyerere, reli ya kisasa ya SGR pamoja na Daraja la Kigongo – Busisi.
“Tuliamua kwanza tumalize miradi mikubwa iliyokuwa imefikia hatua nzuri ili ianze kusaidia uchumi wa nchi. Sasa tunaongeza nguvu kwenye miradi mingine iliyokuwa imepunguza kasi ya utekelezaji wake,” amesema.
Amesema mradi huo wa barabara una umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Kilolo kutokana na eneo hilo kuwa miongoni mwa maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo mkoani Iringa.
Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ujenzi wa barabara hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mikoa na wilaya zinaunganishwa kwa barabara za lami.
Amesema mradi huo umeunganisha Wilaya ya Kilolo na Mkoa wa Iringa kwa urahisi zaidi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kilolo, Rita Kabati amesema wananchi wa Kilolo wameendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya miundombinu huku akiishukuru Serikali kwa kuendelea kutatua changamoto za usafiri katika wilaya hiyo.
“Uchumi wa Kilolo unategemea barabara. Maeneo mengi hayapitiki wakati wa mvua na suluhisho lake ni barabara za lami,” amesema Kabati.
Awali, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa, Mhandisi Hoseat Machaka amesema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 60.14 umefikia asilimia 96 ya utekelezaji na tayari umekabidhiwa kwa matumizi.
Amesema mradi huo umehusisha ujenzi wa Daraja la Ndiwili lenye urefu wa mita 40, makalavati makubwa 13, makalavati madogo 54 pamoja na njia za watembea kwa miguu na waendesha baiskeli kwa lengo la kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Amefafanua kuwa wananchi 596 waliopitiwa na mradi huo walilipwa fidia ya zaidi ya shilingi bilioni 2.54 huku ajira 393 zikizalishwa, ambapo asilimia 95 ya ajira hizo zilitolewa kwa wananchi wa eneo husika.






No comments:
Post a Comment