WIZARA YA ELIMU YAWEKA VIPAUMBELE VITANO KUTEKELEZA DIRA 2050 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 7, 2026

WIZARA YA ELIMU YAWEKA VIPAUMBELE VITANO KUTEKELEZA DIRA 2050



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza vipaumbele vitano vya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027 vitakavyolenga kuimarisha ubora wa elimu, kukuza ujuzi na kuongeza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu nchini.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Prof. Mkenda amesema vipaumbele hivyo vimezingatia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023 ambayo inalenga kuongeza ubora wa elimu na kuendana na mahitaji ya maendeleo ya taifa pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema katika mwaka huo wa fedha, Wizara itaendelea kuweka nguvu katika maandalizi ya utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10, kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na kuongeza matumizi ya TEHAMA katika sekta ya elimu.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kipaumbele cha kwanza kitakuwa kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, kufanya mapitio ya sheria, kuandaa miongozo mbalimbali na kutoa mafunzo nchini.

Aidha, amesema Serikali itaongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo vya amali ili kuwajengea vijana ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa Serikali pia itaendelea kuboresha elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu pamoja na kuongeza ubora wa elimu ya juu nchini.

Katika hatua nyingine, amesema Wizara itaendelea kuimarisha uwezo wa nchi katika tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu ya taifa.

No comments:

Post a Comment