
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB),Bw. Asangye Bangu, amesema WRRB inatarajia kuanza kusimamia uuzwaji wa mifugo kwa kutumia mizani kuanzia Julai 1, 2026, hatua itakayomaliza utaratibu wa muda mrefu wa kuuza mifugo kwa makadirio ya macho.
Bangu ametoa kauli hiyo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, kuanzia Juni 16 hadi 23, 2026.
Amesema matumizi ya mizani katika biashara ya mifugo yataleta uwazi na haki kwa wanunuzi na wauzaji, sambamba na kuhakikisha thamani halisi ya mifugo inapatikana kulingana na uzito wake.
Kwa mujibu wa Bangu, mfumo huo mpya unalenga kuimarisha biashara ya mifugo nchini kwa kuondoa changamoto zinazotokana na upangaji wa bei kwa makadirio, jambo ambalo limekuwa likisababisha malalamiko kwa baadhi ya wadau wa sekta hiyo.
Aidha, amewahimiza wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo kujiandaa kuupokea mfumo huo mpya ambao unatarajiwa kuongeza ufanisi, ushindani na mapato katika biashara ya mifugo nchini.


No comments:
Post a Comment