Mwandishi wetu- Morogoro
Washiriki wa Maonesho ya NANENANE watakiwa kuendelea kuzingatia ubunifu, teknolojia mpya katika shughuli za uzalishaji ili zisaidie katika kutatua changamoto zinazojitokeza.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 08 Agosti, 2026 Mkoani Morogoro na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Prof. Palamagamba Kabudi wakati akifunga maonesho ya NANENANE Kanda ya Mashariki.
Prof. Kabudi amehimiza viongozi wa Mikoa kuhakikisha teknolojia zilizooneshwa kwenye viwanja vya NANENANE zinafikishwa kwa wananchi kupitia huduma za ugani na mashamba darasa.
“Tuendelee kutumia Jukwaa la Business-to-Business (B2B) ili liweze kuweka malengo yanayopimika katika biashara, uwekezaji na masoko” alihimiza Waziri Kabudi.
Aidha, amezitaka taasisi nyingine kama TBS, SIDO ziendelee kujikita katika kuwasaidia wajasiriamali wadogo kufika viwango vinavyohitajika kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utumishi wake wa kipekee katika taifa na kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa alieleza, “Maonesho ya Mwaka yamefanyika yakiwa katika utekelezaji wa mwaka wa kwanza wa Dira ya taifa 2050, nasi tumeondoka katika mafanikio ya maonesho kwa kuangalia idadi ya mabanda na sasa tumeweka vigezo maalumu kwa kuangalia elimu iliyotolewa na teknolojia iliyochukuliwa na muunganiko wa biashara iliyopatikana”.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Batlida Burian amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kusainiwa kwa Mkataba wa Kiwanda cha Usafishaji Mafuta Mkoani Tanga.
“Mhe. Rais ameshaacha tabasamu kabla ya kufika mwaka 2030 mradi huo mkubwa utawezesha kunufaisha Tanga na Kanda nzima ya Mashariki, tumejipanga kuhakikisha kila mtu ananufaika na fursa hii ya ujengwaji wa kiwanda ambayo imetolewa” alibainisha Balozi Batilda.






No comments:
Post a Comment