Serikali imesema maendeleo yanayoonekana kwasasa katika mageuzi ya elimu ni ishara kwamba azma ya kuimarisha elimu ya ujuzi mashuleni imeanza kuzaa matunda, huku wanafunzi wakionesha uwezo mkubwa wa kufanya kazi za vitendo kwa kujiamini.
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 18, 2026 jijini Tanga na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, baada ya kukagua maandalizi ya Mashindano ya Ujuzi 2026 na kutembelea banda la shule za sekondari za mkondo wa amali katika ufunguzi wa Maonesho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara.
Prof. Mkenda amesema wazo la kupeleka ujuzi mashuleni lilianza kusisitizwa na Rais mara tu baada ya kuapishwa, na limeendelea kuwa ajenda muhimu ya mageuzi ya elimu nchini.
"Taswira ya wanafunzi, wakiwemo mabinti wanaowasilisha na kutekeleza kazi za kiufundi kwa umahiri, inaonesha kuwa vijana wanaanza kujenga uwezo wa kujitegemea kupitia elimu inayowaandaa kwa soko la ajira,"amesema.
Aidha, wamesisitiza kuwa taasisi mbalimbali zitaendelea kushirikiana kuandaa mikakati ya kuimarisha mafunzo ya ujuzi ili kuwafikia vijana wengi zaidi na kuendeleza dira ya taifa ya kukuza ubunifu na ajira kupitia elimu ya vitendo.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini China Dkt. Suleiman Haji Suleiman amesema katika maonesho hayo yapo makampuni kutoka China yaliyovutiwa na uwezo wa wanafunzi pamoja na kazi nzuri walizofanya, hivyo wako tayari kutoa ufadhili wa mafunzo kwa wanafunzi hapa Tanzania na pia nchini China.
Amesema baada ya kuhitimu mafunzo watawapokea kwa ajira moja kwa moja katika makampuni yao, pamoja na kuwasaidia kupata fursa katika makampuni mengine ya China yanayofanya kazi Tanzania na yanayohitaji wataalamu wenye ujuzi wa teknolojia hizo.
"Ujumbe walionipa ni kwamba kupitia Wizara ya Elimu au Ofisi ya Mkuu wa Mkoa liandaliwe andiko maalum litakaloeleza namna ya utekelezaji, wapi pa kuanzia, wanafunzi wangapi wachukuliwe kila mwaka, na jinsi programu hiyo itakavyotekelezwa,"amesema.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo amesema kupitia mpango huo kila mwanafunzi ana nafasi ya kupata elimu kulingana na uwezo wake wakiwemo wenye mahitaji maalum.
"Mkakati huu unatekelezwa katika ngazi zote kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari hadi vyuo vikuu, elimu maalum inapewa kipaumbele kupitia walimu wenye ujuzi wa lugha ya alama, utoaji wa vifaa saidizi na mazingira rafiki ya kujifunzia, ili vijana wa Tanzania waweze kutimiza ndoto zao,"amesema.
Maonesho hayo yamefunguliwa leo Agosti 18 na Prof. Mkenda ambapo yanatarajiwa kuhitimishwa Agosti 24,2026.







No comments:
Post a Comment