DKT. MWIGULU AIPONGEZA TANESCO KUTUMIA WATAALAMU WA NDANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 15, 2026

DKT. MWIGULU AIPONGEZA TANESCO KUTUMIA WATAALAMU WA NDANI


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewapongeza viongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuhakikisha Kituo cha Kupokea, Kupooza na Kusambaza Umeme cha Imalilo pamoja na njia ya kusafirisha umeme kutoka Shinyanga hadi Simiyu vinaendelea kujengwa kwa kutumia wataalamu wa ndani.

"Hongereni sana TANESCO kwa uamuzi wenu wa kutekeleza ujenzi wa kituo hiki kwa kutumia wataalamu wa ndani baada ya changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mkataba na mkandarasi wa awali lakini pia niwapongeze na kazi mnayofanya. Ni nzuri. Ina standard na ubora," amesema.

Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo leo (Jumanne, Septemba 15, 2026) baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Imalilo na kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, na kuongeza kuwa hatua hiyo imeonesha uwezo wa wataalamu wa Kitanzania katika kutekeleza miradi mikubwa kwa viwango vinavyostahili.

Waziri Mkuu ambaye yuko katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu, ameiagiza TANESCO iongeze kasi ya utekelezaji wa Mradi wa Gridi Imara mkoani Simiyu na kuhakikisha Kituo cha Imalilo pamoja na njia ya kusafirisha umeme kutoka Shinyanga hadi Simiyu vinakamilika kwa wakati.

Amesema Serikali itahakikisha mtiririko wa fedha unaendelea ili kukamilisha njia hiyo ya kusafirisha umeme, akisisitiza kuwa kukamilika kwa kituo cha Imalilo bila kukamilika kwa njia ya kuleta umeme hakutatatua changamoto ya upatikanaji wa umeme mkoani Simiyu. "Fedha zipo, kazi ifanyike. Fanyeni kazi mchana na usiku ili kazi hii iishe kwa wakati," amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema eneo linalohitaji msukumo mkubwa sasa ni kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme kutoka Ibadakuli, Shinyanga hadi Imalilo yenye urefu wa kilomita 110, ili kituo hicho kiweze kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa. "Tutasukuma fedha kwenye njia ya kuleta umeme ili seti yote iweze kukamilika. Tukiweka tu transforma hapa bila kuwa na njia ya kuleta umeme tutakuwa bado hatujamaliza," amesema.

Amesema Simiyu ni mkoa wa kimkakati kwa uwekezaji katika viwanda kutokana na nafasi yake kijiografia na rasilimali zilizopo, hivyo kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuimarisha upatikanaji na ubora wa umeme pamoja na kuwezesha shughuli za kiuchumi. "Kilio cha kukatika katika umeme ni kikubwa sana. Na Simiyu ni mkoa wa kimkakati kwenye viwanda," amesema.

Waziri Mkuu amesema baada ya kurejea Dodoma atafanya kikao na Wizara ya Nishati na Wizara ya Fedha ili kuhakikisha mtiririko wa fedha haukwamishi utekelezaji wa mradi huo, huku akiwaagiza wakandarasi waongeze kasi ya kazi na kuhakikisha timu nzima inakuwa eneo la mradi wakati wote.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange amesema Kituo cha Imalilo kinajengwa kwa fedha za ndani kwa gharama ya sh. bilioni nane na hadi Septemba 13, 2026 utekelezaji wake umefikia asilimia 82.

Bw. Twange amesema TANESCO iliamua kutekeleza mradi wa kituo hicho chenye uwezo wa MVA 60, kV 220/33, kwa kutumia wataalamu wake wa ndani baada ya kutokukubaliana na masharti ya utekelezaji ya kampuni ya Xian Electric Engineering Company Limited iliyokuwa imepewa kazi hiyo awali.

Amesema njia ya kusafirisha umeme kutoka Ibadakuli, Shinyanga hadi Imalilo yenye urefu wa kilomita 110 na msongo wa kV 220 inagharimu sh. bilioni 48.7, huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 60 na unatarajiwa kukamilika Februari, 2027.

Bw. Twange amesema mkandarasi ameshapeleka eneo la mradi takribani asilimia 90 ya vifaa vinavyohitajika na kazi za ujenzi wa misingi zimefikia zaidi ya asilimia 50, huku changamoto kubwa ikiwa ni upatikanaji wa fedha za kumlipa mkandarasi na wakandarasi wadogo.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa njia hiyo, mwakilishi mkazi wa kampuni ya Kalpataru Project International ya India, Bw. Ashish Tehran alisema ujenzi wa misingi umefikia asilimia 50 na ujenzi wa minara umeanza, huku vifaa vya mradi vikiwa vimewasili eneo la kazi.

Amesema pamoja na changamoto zilizopo katika baadhi ya misingi, wanaendelea na kazi na wanaamini watakamilisha mradi kwa wakati. Mradi huo pia unatarajiwa kutoa ajira kwa wananchi wa maeneo yanayotekelezwa, ikiwemo takribani ajira 200 kwa wakazi wa eneo la Bunamhala.DKT. MWIGULU AIPONGEZA TANESCO KUTUMIA WATAALAMU WA NDANI

No comments:

Post a Comment