TARURA YAONDOA ADHA YA USAFIRI KWA WANANCHI WA KIJIJI CHA SONGE WILAYANI KILINDI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, November 23, 2026

TARURA YAONDOA ADHA YA USAFIRI KWA WANANCHI WA KIJIJI CHA SONGE WILAYANI KILINDI


‎Na Mwandishi Wetu - Kilindi, Tanga
‎

‎Wananchi wa kijiji cha Songe kata ya Songe wilaya ya Kilindi mkoani Tanga wanatarajia kuondokana na adha ya usafiri kufuatia ujenzi wa barabara ya Polisi yenye urefu wa mita 650 kwa kiwango cha lami mradi unaotekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
‎
‎Mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 315 fedha kutoka Mfuko wa Barabara ulianza kutekelezwa Februari 6, 2026 na unatarajiwa kukamilika Desemba 16, 2026 ambapo kwa sasa kazi zinazoendelea ni uwekaji wa lami pamoja na ujenzi wa mifereji ya kupitisha maji ya mvua ili kuhakikisha barabara inakuwa imara na inapitika kwa urahisi katika misimu yote.
‎
‎Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Dickson Mugisha kutoka TARURA wilaya ya Kilindi amesema kukamilika kwa barabara hiyo itakuwa suluhisho ya changamoto ya muda mrefu ya usafiri kwa wananchi wa Kata ya Songe.
‎
‎Amesema barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kwa kuwa inaunganisha wananchi na huduma muhimu za kijamii ikiwemo Kituo cha Polisi, Stendi ya Wilaya, Kituo cha Afya pamoja na shule za msingi na sekondari.
‎
‎Ameongeza kuwa ujenzi huo utafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali, kupunguza gharama za usafiri na kuongeza kasi ya shughuli za maendeleo katika eneo hilo.
‎
‎"Mradi huu utakapokamilika, wananchi watanufaika kwa kupata huduma mbalimbali kwa urahisi na tunaishukuru serikali kwa kutupatia fedha ili kutekeleza mradi huu", amesema Mhandisi Mugisha.
‎
‎Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Songe Bw. Said Ramadhani amesema barabara hiyo ilikuwa katika hali mbaya kwa zaidi ya miaka 10 hali iliyokuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi hususan wakati wa mvua.
‎
‎Ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami utabadilisha muonekano wa kijiji hicho na kuimarisha usafiri pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii.
‎
‎Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali katika kulinda miundombinu hiyo kwa kuepuka kutupa taka kwenye mifereji ya maji ya mvua ili kuzuia kuziba kwa mitaro na kusababisha mafuriko yanayoweza kuharibu barabara.
‎
‎Naye, Bw. Ally Omari mkazi wa Songe ameishukuru serikali kupitia TARURA kwa kutekeleza mradi huo akisema awali hasa wakati wa mvua ilikuwa vigumu kufika hospitalini na kituo cha polisi kutokana na hali mbaya ya barabara.
‎
‎"Barabara hii ilikuwa changamoto wakati wa mvua tulipata shida kufika hospitalini au kituo cha polisi lakini sasa tunaona matumaini ya kupata huduma hizo kwa wakati na bila usumbufu", amesema Omari.
‎
‎Kwa upande wake, Bi. Mwajuma Kisiki mkazi mwingine wa Songe amesema hali ya barabara hiyo wakati wa mvua ilikuwa mbaya kiasi cha kushindwa kupitika kwa watembea kwa miguu na hata magari.
‎
‎Amesema ujenzi unaoendelea umeanza kuleta matumaini mapya kwa wananchi kwani sasa wanatarajia kuwa na barabara itakayowawezesha kusafiri na kusafirisha mazao yao bila vikwazo vya hali ya hewa.

No comments:

Post a Comment