WANANCHI MKOANI MBEYA WAFURAHIA KUREJEA KWA HUDUMA YA UMEME - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, November 23, 2026

WANANCHI MKOANI MBEYA WAFURAHIA KUREJEA KWA HUDUMA YA UMEME


Na Mwandishi Wetu, Mbeya


Wananchi mbalimbali mkoani Mbeya wameeleza kufurahishwa na kurejea kwa huduma ya umeme usiku wa kuamkia Novemba 23, 2026, baada ya kukatika kufuatia kuanguka kwa mnara wa njia ya kusafirisha umeme ya Mradi wa TAZA katika eneo la Inyala.

Kurejea kwa huduma hiyo kumewawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku, hususan biashara zilizokuwa zimeathiriwa na kukosekana kwa umeme.

Akizungumza kuhusu kurejea kwa huduma hiyo, mkazi wa Soweto, Victor Mkini, ameishukuru TANESCO kwa juhudi za kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha umeme unarejea.

“Tunawashukuru TANESCO kwa juhudi zao za kuhakikisha umeme unarejea. Walikuwa wakitupatia taarifa kuhusu hatua zilizokuwa zikichukuliwa hadi huduma iliporejea,” amesema Mkini.

Kwa upande wake, Lilian Kalugha amesema kukatika kwa umeme kuliathiri shughuli zao za kibiashara kwa kuwa zinategemea zaidi huduma hiyo, huku akiishukuru TANESCO kwa kuendelea kutoa taarifa na ushirikiano wakati wote wa changamoto hiyo.

Naye Hekima Kadogo amesema kukatika kwa umeme kulisimamisha shughuli mbalimbali, lakini ameeleza kuridhishwa na namna TANESCO ilivyokuwa ikitoa taarifa kuhusu maendeleo ya jitihada za kurejesha huduma hiyo.

Amesema utoaji wa taarifa kwa wananchi uliwasaidia kufahamu hatua zilizokuwa zikichukuliwa katika kutatua changamoto hiyo.

Kukatika kwa umeme kulitokana na kuanguka kwa mnara wa njia mpya ya kusafirisha umeme ya kilovolti 400 ya Mradi wa TAZA katika eneo la Inyala, Novemba 21, 2026, hali iliyosababisha kuathirika kwa miundombinu ya njia ya kilovolti 220 inayosafirisha umeme kutoka Iringa kwenda Mbeya. 

Kufuatia tukio hilo, TANESCO iliendelea na jitihada za kurejesha huduma kwa kufanya kazi usiku na mchana, hatua iliyowezesha umeme kurejea katika mikoa ya Mbeya na Songwe usiku wa kuamkia Novemba 23, 2026.

No comments:

Post a Comment