NA MWANDISHI WETU - DODOMA
Tume ya Madini imeeleza dhamira yake ya kuimarisha mikakati na mifumo ya kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na uenezaji wa silaha za maangamizi katika sekta ya madini, kwa kusisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya taasisi za udhibiti ili kuongeza ufanisi katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kifedha nchini.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Eng. Hamisi Kamando, aliyemwakilisha Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Eng. Ramadhani Lwamo, wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 12 cha Jukwaa la Wasimamizi wa Masuala ya Kupambana na Utakatishaji Fedha Haramu, Ufadhili wa Ugaidi na Uenezaji wa Silaha za Maangamizi (AML/CFT/CPF), kinachofanyika Novemba 26–27, 2026, katika Ukumbi wa Graphite, Makao Makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, Eng. Kamando amesema maandalizi ya Awamu ya Tatu ya Tathmini ya Kikundi cha Kupambana na Utakatishaji Fedha Haramu Afrika Mashariki na Kusini (ESAAMLG) yanahitaji ushirikiano wa karibu baina ya taasisi, akibainisha kuwa tathmini hiyo haitazingatia uwepo wa sheria, kanuni na taratibu pekee, bali pia ufanisi wa utekelezaji wake na matokeo yanayopatikana katika kudhibiti uhalifu wa kifedha.
Amesisitiza umuhimu wa kila taasisi kutambua wajibu wake, kubaini maeneo yenye changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utekelezaji wa majukumu yake, sambamba na kuhakikisha kunakuwepo na taarifa na ushahidi wa kutosha unaothibitisha hatua zinazochukuliwa kudhibiti vihatarishi vya utakatishaji fedha haramu.
Akizungumzia sekta ya madini, amesema Tume ya Madini inaendelea kutambua umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini yenye thamani na madini ya vito, hususan katika kudhibiti biashara haramu, utoroshaji wa madini na miamala yenye viashiria vya kutia shaka.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Tume ya Madini, Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) na mamlaka nyingine za udhibiti ni muhimu katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na uadilifu katika biashara ya madini nchini.
Aidha, Eng. Kamando ameishukuru FIU kwa kuendelea kuratibu ushirikiano baina ya taasisi katika kuimarisha mifumo ya kudhibiti uhalifu wa kifedha, akieleza matumaini yake kuwa majadiliano ya jukwaa hilo yatawezesha kubainisha mikakati na hatua madhubuti za kuboresha utendaji wa taasisi zinazohusika.
Kikao hicho cha siku mbili kinalenga kujadili utekelezaji wa Mkakati na Mpango Kazi wa Kitaifa wa AML/CFT/CPF, maandalizi ya tathmini ya ESAAMLG pamoja na masuala yanayohusu usimamizi wa biashara na taaluma zisizo za kifedha (DNFBPs).
Jukwaa hilo limewakutanisha wawakilishi wa FIU, mamlaka za udhibiti na taasisi mbalimbali za umma kwa lengo la kuimarisha uratibu, ushirikiano na ufanisi katika mapambano dhidi ya utakatishaji fedha haramu na uhalifu mwingine wa kifedha nchini.






No comments:
Post a Comment