
Watumishi wa Jeshi la Magereza mkoa wa Kigoma, tarehe 25 Septemba, 2025 wamepokea majiko ya gesi ya sahani mbili pamoja na mitungi yake ya kilo 15 zaidi ya 398 kutoka kwa Msambazaji kampuni ya ORYX Tanzania kwa uwezeshaji wa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ikiwa ni jitihada za Serikali ili kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akipokea majiko hayo pamoja na mitungi yake Mkuu wa Magereza ya mkoa wa Kigoma Kamishna Msaidizi (ACP); Isani Mjimbi ameishukuru Serikali kwa kufikisha teknolojia za nishati safi ikiwemo majiko ya gesi ya sahani mbili pamoja na mitungi yake ya kilo 15 na kuongeza kuwa askari wa Magereza watayatumia na kuwa mabalozi wa nishati safi kwa Wananchi wengine.
“Ninaahidi kwa niaba ya Watumishi wa Magereza kuwa, tutayatumia majiko haya na tutakuwa mabalozi kwa Wananchi wengi katika kutumia gesi kama chanzo cha nishati safi ya kupikia, majumbani mwetu” alisema Kamishna Mjimbi.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Mhandisi, Ahmed Chinemba amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kuwezesha, kuhamasisha na kutoa elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Wananchi wakiwemo Watumishi wa Magereza ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024/2034 ambao unasisitiza angalau asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishari safi ya kupikia ifikapo 2034
“Tukio la leo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia na ni matumaini yetu kuwa baada ya Serikali kusambazia Magereza majiko haya pamoja na mitungi ya gesi, watafikiwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) pamoja na Taasisi zingine” alisema Mhandisi, Chinemba.
REA kwa kushirikia na Magereza wamendelea kuwafikia Watumishi wa Jeshi hilo ambapo leo ilikuwa ni zamu ya mkoa wa Kigoma ambapo jumla ya majiko ya gesi na mitungi yake 398 imeanza kusambazwa mkoani humo ambapo usambazaji umezinduliwa rasmi katika Gereza la Kigoma Makao Makuu na Gereza la wilaya la Bangwe.







No comments:
Post a Comment