NIDHAMU, UWAZI NA UFANISI VITAWALE SEKTA YA UJENZI – ULEGA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 30, 2026

NIDHAMU, UWAZI NA UFANISI VITAWALE SEKTA YA UJENZI – ULEGA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG – Dodoma


Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kuongeza uwajibikaji, ufanisi na nidhamu ya kazi ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Akizungumza Machi 30, 2026 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi, Ulega alisisitiza umuhimu wa taasisi hizo kuwasilisha kwa wakati taarifa za utendaji wa bodi zao. Alibainisha kuwa, kwa mujibu wa sheria, taarifa hizo zinapaswa kuwasilishwa miezi mitatu kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha.

Aidha, Waziri huyo amewataka viongozi wa taasisi zinazotekeleza mageuzi mbalimbali kuongeza kasi ya utekelezaji ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Alitolea mfano Wakala wa Majengo Tanzania, akieleza kuwa umeelekezwa kuandaa mpango wa biashara (Business Plan) utakaoiwezesha taasisi hiyo kujiendesha kibiashara.

Katika hatua nyingine, aliielekeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuongeza juhudi katika kusimamia miradi ya miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Pia, amezitaka taasisi zinazokusanya maduhuli zikiwemo AQRB, ERB na CRB kuongeza makusanyo pamoja na kudhibiti matumizi ili kuimarisha ufanisi na tija ya taasisi hizo.

Mbali na hilo, Waziri Ulega amewakumbusha viongozi hao kuzingatia maadili ya uongozi wa umma kwa kupiga vita rushwa, kuheshimu utawala wa sheria na kutunza siri za ofisi, akisisitiza kuwa nafasi walizonazo ni dhamana kwa wananchi.

“Ni wajibu wenu kuhakikisha mnasimamia rasilimali za umma kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu ili kuendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwaletea wananchi maendeleo,” amesisitiza Ulega.

Kadhalika, amesisitiza umuhimu wa kuitisha mabaraza ya wafanyakazi katika taasisi zote ili kuimarisha mahusiano kati ya menejimenti na watumishi, akibainisha kuwa bado kuna malalamiko kutoka kwa baadhi ya watumishi.

Waziri Ulega amewataka watumishi wa sekta ya ujenzi kufanya kazi kwa bidii, weledi na kuepuka vitendo vya rushwa pamoja na matumizi mabaya ya ofisi, ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.





No comments:

Post a Comment