FITCH YAITHIBITISHIA TANZANIA DARAJA LA ‘B+’, MTAZAMO WAENDELEA KUWA THABITI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 30, 2026

FITCH YAITHIBITISHIA TANZANIA DARAJA LA ‘B+’, MTAZAMO WAENDELEA KUWA THABITI


Na Joseph Mahumi, WF


Kampuni ya tathmini ya nchi kukopa na kulipa mikopo ya Fitch Ratings, imeithibitisha Tanzania kuendelea kuwa ‘B+’ huku likidumisha mtazamo wa “Stable Outlook”. Hatua hiyo inaashiria imani ya Kampuni hiyo katika mwenendo wa uchumi wa nchi pamoja na uthabiti wake wa kifedha katika kipindi cha kati.

Kwa mujibu wa tathmini hiyo, Tanzania inaendelea kunufaika na ukuaji mzuri wa pato la taifa (GDP) , kiwango cha chini cha mfumuko wa bei, deni kuendelea kuwa himilivu ikilinganishwa na nchi nyingine zinazofanana.

Mwenendo mzuri wa uchumi umepelekea upatikanaji wa fedha za nje kupitia programu za Shirika la Fedha la Kimataifa - IMF ikiwemo Extended Credit Facility (ECF) inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii na Resilience Sustainability Facility (RSF) ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti hiyo pia imeeleza kuwa ushindi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi wa Oktoba 2025 unatarajiwa kuendeleza sera za kiuchumi, jambo litakalosaidia utekelezaji wa mipango ya mageuzi ya uchumi na kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji.

Kwa upande wa ukuaji wa uchumi, Fitch inatarajia Tanzania kuendelea kuwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 6 mwaka 2026 na 2027, juu ya wastani wa nchi zilizo katika kundi la ‘B’ ambapo Ukuaji huo utachangiwa na sekta za kilimo na madini pamoja na uwekezaji mkubwa katika miundombinu, ikiwemo mradi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway na bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Kwa upande wa sera za fedha za umma, Fitch inakadiria nakisi ya bajeti kubaki karibu asilimia 3 ya Pato la Taifa katika miaka ya fedha 2026 na 2027, huku ukusanyaji wa mapato ukiendelea kuimarika kutoka asilimia 14.2 ya Pato la Taifa mwaka wa fedha 2021 hadi asilimia 15.9 mwaka wa fedha 2025.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa Mapato ya utalii (travel exports) yalifikia dola za Marekani bilioni 4.4 mwaka 2025, sawa na asilimia 25 ya mauzo yote ya bidhaa na huduma nje ya nchi.

Hata hivyo, hali hii itafidiwa kwa kiasi na kuongezeka kwa thamani ya mauzo ya dhahabu ya Tanzania nje ya nchi, ambayo yalifikia dola za Marekani bilioni 4.7 mwaka 2025 (sawa na asilimia 27 ya jumla ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi).

Aidha, deni la serikali linatarajiwa kushuka hadi asilimia 47 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2027, likisaidiwa na ukuaji wa uchumi na nidhamu ya matumizi ya Serikali.

Tathmini hiyo pia imepongeza jitihada za Serikali katika kuboresha usimamizi wa fedha za umma, ikiwemo kupunguza madeni ya wazabuni na marejesho ya VAT katika miaka ya karibuni ambapo Kufikia Desemba 2025, kiasi kilichothibitishwa cha madeni hayo kilipungua hadi asilimia 0.2 ya Pato la Taifa (GDP), kutoka asilimia 1.2 mwishoni mwa Desemba 2022, hatua inayochangia kuongeza uwazi na ufanisi wa kifedha.

“Ninawapongeza Viongozi wa Wizara Taasisi zake zote waliofanikisha kazi ya kusimamia sekta hii ya uchumi na fedha, tunafarijika kuona matokeo haya ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu kwani tutaendelea kuaminika katika masoko ya fedha na dhamana ya Kimataifa” alisema Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha

Kwa ujumla, uthibitisho wa daraja la ‘B+’ na mtazamo thabiti unaashiria kuwa Tanzania inaendelea kujenga msingi imara wa uchumi, huku ikiongeza imani ya wawekezaji wa ndani na kimataifa katika uwezo wa nchi kusimamia uchumi wake na kukabiliana na mishtuko ya nje.

No comments:

Post a Comment