TEKNOLOJIA NA RASILIMALI ZATAJWA KUHITAJI HATUA ZA HARAKA KATIKA SEKTA YA NISHATI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 30, 2026

TEKNOLOJIA NA RASILIMALI ZATAJWA KUHITAJI HATUA ZA HARAKA KATIKA SEKTA YA NISHATI

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SEKTA binafsi imeelezwa kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo (FYDP IV), huku Serikali ikisisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wake katika uwekezaji wa nishati ili kufikia uzalishaji wa megawati 70,000 ifikapo mwaka 2050.

Hayo yamebainishwa Machi 30, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la kitaifa kuhusu ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) katika sekta ya nishati, lililolenga kujadili nafasi ya sekta binafsi katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika chini ya Mpango wa Nne wa Maendeleo.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPPC), David Kafulila, alisema sekta binafsi ni mhimili muhimu katika utekelezaji wa mpango huo, ambao ni sehemu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alifafanua kuwa rasilimali za Serikali pekee, zikiwemo mapato ya kodi na mikopo, hazitoshi kufikia lengo la uzalishaji wa umeme unaotarajiwa kufikia takribani megawati 70,000 ifikapo mwaka 2050.

Kutokana na hali hiyo, alisisitiza umuhimu wa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uwekezaji wa miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme ili kuongeza kasi ya maendeleo ya sekta hiyo.

Kafulila alieleza kuwa licha ya kuwepo kwa vikwazo vya kisheria vinavyozuia baadhi ya aina za ubia katika sekta ya usafirishaji wa umeme, Serikali imeanza hatua za majaribio kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na kampuni binafsi, ili kuanzisha mradi wa kwanza wa aina hiyo.

Aliongeza kuwa hatua hiyo inalenga kupima ufanisi wa ubia huo, sambamba na kutoa fursa ya kuboresha mifumo ya kisheria ili kuruhusu ushiriki mpana zaidi wa sekta binafsi katika siku zijazo.

Kwa upande wake, Balozi Modest Mero alisisitiza umuhimu wa kuimarisha maadili na mtazamo mpana miongoni mwa wadau wa sekta za umma na binafsi ili kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa manufaa ya umma.

Alionya kuwa kutokuzingatia hilo kunaweza kusababisha maamuzi yanayoweka mbele maslahi binafsi badala ya maendeleo ya wananchi, akihimiza hatua za haraka zichukuliwe kukabiliana na changamoto za teknolojia na rasilimali.

Naye mtaalamu wa uchumi, Dkt. Avit Mushi, alisema sekta binafsi ina nafasi kubwa ya kuharakisha maendeleo kutokana na ufanisi wake, akisisitiza umuhimu wa taasisi na watumishi kuwa na mtazamo chanya wa kufanikisha malengo ya maendeleo ili kuongeza tija.

No comments:

Post a Comment