SERIKALI YAIMARISHA HAKI NA FURSA KWA WATU WENYE DOWN SYNDROME - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, March 25, 2026

SERIKALI YAIMARISHA HAKI NA FURSA KWA WATU WENYE DOWN SYNDROME



Na Okuly Julius, OKULY BLOG Dodoma


Serikali imeendelea kuonesha dhamira thabiti ya kuhakikisha watu wenye Down Syndrome wanapata haki, huduma bora na fursa sawa katika nyanja zote za maisha, sambamba na kuhamasisha jamii kuwa na mtazamo chanya na jumuishi kwa kundi hilo muhimu katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza jijini Dodoma kuhusiana na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Down Syndrome inayoadhimishwa kila mwaka Machi 21, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Kizito Wambura, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kundi hilo haliachwi nyuma.

Amesema hatua hizo ni pamoja na kuweka mifumo madhubuti ya kisheria na kisera ikiwemo Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, Sera ya Maendeleo ya Watu wenye Ulemavu pamoja na Sera ya Elimu na Mafunzo, kwa lengo la kulinda haki na ustawi wao.

Aidha, Wambura amesisitiza kuwa watu wenye Down Syndrome wana mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kupitia sekta mbalimbali kama elimu, sanaa, michezo na shughuli za kijamii na kiuchumi, hivyo jamii inapaswa kuwatambua, kuwaheshimu na kuwawezesha kikamilifu.

Kwa upande mwingine, Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku hiyo iliyoidhinishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2011 kwa lengo la kuongeza uelewa na kutambua mchango wa watu wenye hali hiyo.

Kwa mwaka huu, viongozi wa kitaifa wa chama cha watu wenye Down Syndrome wanatarajiwa kukutana Moshi, mkoani Kilimanjaro, huku kaulimbiu isemayo “Tuwe Pamoja Dhidi ya Upweke” ikilenga kuhamasisha mshikamano na ushirikishwaji wao katika jamii.

Siku hii pia hutambua mchango wa Dkt. Langdon Down aliyegundua hali hiyo, huku ikiendelea kuhimiza jamii kuheshimu haki za watu wenye Down Syndrome ikiwemo haki ya elimu, ajira, huduma za afya pamoja na ushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa, watu wenye Down Syndrome wanastahili kuishi kwa kujitegemea ndani ya jamii, kupata elimu jumuishi, kushiriki katika ajira na kushiriki kikamilifu katika utamaduni, michezo na burudani.



No comments:

Post a Comment