TANZANIA YAADHIMISHA SIKU YA IORA KWA KUPANDA MITI MTUMBA NA KUFANYA MAZOEZI MEPESI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, March 7, 2026

TANZANIA YAADHIMISHA SIKU YA IORA KWA KUPANDA MITI MTUMBA NA KUFANYA MAZOEZI MEPESI


Tanzania imeungana na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Bahari ya Hindi (IORA) kuadhimisha miaka 29 ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo katika hafla iliyofanyika katika mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma ambapo miti ya Matunda na Kivuli imepandwa.

Akiongoza maadhimisho hayo, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira Balozi Baraka Luvanda ameshiriki mazoezi mepesi na upandaji miti ya matunda na kivuli uliofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikiwa ni ishara ya utunzaji wa mazingira na kuimarisha afya za washiriki.


Akizungumza katika maadhimisho hayo, Balozi Luvanda ameeleza namna nchi inavyonufaika na IORA kupitia Jitihada za pamoja za kuhakikisha rasilimali za Bahari ya Hindi zinatumika kwa maendeleo endelevu na kuongeza kuwa Jumuiya hiyo inawawezesha nchi wanachama kukusanya nguvu na kukabiliana na changamoto mbalimbali kwa pamoja.

Pia ameeleza kuwa kupitia jumuiya hiyo nchi wanachama zimekuwa zikipambana na uvuvi haramu, kutangaza fursa zinazopatikana katika bahari ya Hindi hususani uchumi wa buluu, kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo kwa watalaam wa nchi wananchama na kutoa wito kwa wadau kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za IORA na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya Jumuiya hiyo.

Ameeleza kuwa zoezi la upandaji miti lililofanyika linaunga mkono maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia kampeni ya “27 ya Kijani”.

“Hii pia ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la 2024) na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambazo kwa pamoja zinatilia mkazo uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu dhidi ya changamoto za kiikolojia,” alisisitiza Balozi Luvanda.

Maadhimisho hayo yamefanyika chini ya kauli mbiu isemayo “IORA INABORESHA MAISHA” (IORA Improves Lives), ikilenga kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa Jumuiya hiyo kwa jamii za nchi wanachama.

No comments:

Post a Comment