GAVANA BoT: TUDUMISHE AMANI, UZALENDO NA USHIRIKIANO KATIKA KUJENGA UCHUMI WETU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, March 7, 2026

GAVANA BoT: TUDUMISHE AMANI, UZALENDO NA USHIRIKIANO KATIKA KUJENGA UCHUMI WETU



Katika kuadhimisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, Benki kuu ya Tanzania (BoT) iliandaa hafla maalum ya futari jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mahusiano na wadau wake.

Hafla hiyo iliyofanyika tarehe 6 Machi 2026 ilihudhuriwa na viongozi wa dini, viongozi wa serikali, viongozi wa mabenki na taasisi za fedha nchini pamoja na watu wenye mahitaji maalum.

Akizungumza katika hafla hiyo, Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba amewataka watanzania wote kudumisha amani, uzalendo na ushirikiano katika kujenga uchumi wa Tanzania.

“Naomba tuendelee kuliombea taifa letu amani, upendo na mshikamano. Tuendelee kudumisha uzalendo na ushirikiano katika kujenga uchumi wetu, hasa katika kipindi hiki ambacho uchumi wa dunia unakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo mivutano ya kisiasa na misukosuko ya kiuchumi”.

Pia, katika hafla hiyo Gavana aliwaeleza washiriki kuwa uchumi umeendelea kuimarika, sekta ya fedha iko imara, yenye mtaji na ukwasi wa kutosha, inayojiendesha kwa ufanisi na faida, na inayokua kwa kasi ya kuridhisha.

“Mwaka 2025, uchumi wa Tanzania ulikua kwa takriban asilimia 6, huku Zanzibar uchumi ukikua kwa asilimia 6.8. Mwaka 2026, ukuaji unatarajiwa kufikia asilimia 6.3 kwa Tanzania Bara na asilimia 7.2 kwa Zanzibar.”, alieleza Gavana huyo.

Alisema kuwa ukuaji huo wa uchumi umechochewa na kuimarika kwa shughuli za kilimo, upatikanaji wa umeme wa uhakika, mazingira bora ya biashara, kuongezeka kwa mauzo ya nje hususan dhahabu na kahawa, pamoja na ongezeko la watalii nchini.

Awali, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir aliipongeza Benki Kuu kwa kuandaa hafla hiyo akiitaja kuwa ni ishara tosha kwamba BoT inathamini umoja na inaamini katika kuwaleta Watanzania pamoja bila kujali tofauti za kidini au kijamii.

“Hatua hii ya Benki Kuu ya Tanzania inaonyesha kuwa katika taifa letu hakuna ubaguzi; sisi sote ni Watanzania, tunashirikiana kujenga nchi yetu, na tunapaswa kuendelea kuimarisha mshikamano huo kwa manufaa ya taifa letu”.

Alisema katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje BAKWATA, Sharif Tahir Almusawa.






No comments:

Post a Comment