Tanzania imesisitiza dhamira yake kuendeleza ushirikiano wa kikanda katika usimamizi wa rasilimali za maji katika Mkutano wa Maji wa Sululta na Diplomasia ya Maji (Sululta Water and Hydro Diplomacy Conference) uliofanyika katika Mji wa Bishoftu, nchini Ethiopia.
Mkurugenzi wa Ubora wa Maji, Bw. Heri Chisute kwa niaba ya Waziri wa Maji, amesema mkutano huo wenye kaulimbiu “Diplomasia ya Maji na Ushirikiano wa Kikanda kwa Maendeleo Endelevu ya Maji na Nishati pamoja na Usimamizi Wake” unakumbusha maji ni zaidi ya rasilimali. ni uhai, daraja linalounganisha mataifa na msingi wa amani na ustawi.
“Kwa Tanzania ushirikiano wa kikanda wa majishirikishi ni ushuhuda unaoishi; kutoka Bonde la Mto Nile hadi Kamisheni ya Bonde la Mto Zambezi, Kamisheni ya Bonde la Mto Songwe hadi Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, tumejifunza kwamba mataifa yanaposhirikiana kwenye eneo la majishirikishi, maji huwa chanzo cha umoja badala ya mgogoro”, Chisute amesema.
Ameongeza Tanzania imejikita katika misingi mitatu mikuu katika kushughulikia suala la rasilimali za maji. Mosi, usawa na ujumuishi ambapo ni muhimu kuhakikisha kila jamii, iliyo juu au chini ya chanzo cha maji, inaheshimiwa na kushirikishwa katika maamuzi yanayoathiri maisha na ustawi wao.
Pili, uendelevu na uwajibikaji kwenye kutunza rasilimali za maji ambazo sio toshelevu, hivyo zinapaswa kusimamiwa vizuri na kutumika kwa uangalifu kwa mahitaji ya sasa na vizazi vijavyo.
Tatu, diplomasia na ushirikiano ambapo amefafanua kuwa diplomasia ya maji sio tu suala la kiufundi; bali ni kujenga uaminifu, kukuza wigo wa majadiliano na kukuza ushirikiano baadala ya ushindani.
“Tanzania na Ethiopia zimekuwa na historia ndefu ya uhusiano mzuri na urafiki wa kudumu, sio tu katika diplomasia ya maji bali pia katika nyanja zote za ushirikiano wa kikanda. Matarijio ni kuwa mkutano huu utakuwa alama nyingine ya hatua muhimu katika safari yetu ya pamoja kuelekea utawala endelevu wa maji, mshikamano wa kikanda na kuimarishwa kwa urafiki wa kudumu kati ya Tanzania na Ethiopia”, Chisute ameeleza.
Ametoa wito kwa nchi za Afrika kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha rasilimali za maji zinakuwa chanzo cha maendeleo endelevu na mshikamano wa kikanda. “Wanachi wetu hawataki tu maneno, hivyo, tujitahidi kuunda mifumo iliyo wazi, jumuishi na inayotekelezeka. Tuhakikishe kwamba diplomasia ya maji inakuwa nuru ya umoja wa Afrika na mfano kwa dunia nzima", Chisute amesisitiza.
Mkutano huo umehusisha mijadala mbalimbali ikiwa ni pamoja na hoja ya uanzishwaji wa mifumo imara ya maamuzi inayotegemea kuongeza ushirikiano kati ya taasisi za utafiti na kuhamasisha ushiriki wa vyombo vya habari katika kuelimisha umma kuhusu diplomasia ya maji kwa lengo la kuongeza uelewa.
Mkutano huo uliopangwa kufanyika mara mbili kwa mwaka umeandaliwa na Wizara ya Maji na Nishati ya nchini Ethiopia kwa kushirikiana na taasisi ya African Leadership Excellence Academy (AFLEX). Lengo likiwa kuwa jukwaa muhimu la kujadili masuala nyeti ya maji na kukuza ushirikiano wa kikanda kwa nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile.
Mkutano umewakutanisha Mawaziri, watunga sera na wataalamu kutoka nchi wanachama wa bonde la mto Nile ili kubadilishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano na kuendeleza mbinu shirikishi katika usimamizi wa rasilimali za maji zinazovuka mipaka.
Diplomasia ya maji inamaanisha matumizi ya mazungumzo na ushirikiano wa kisiasa katika kusimamia rasilimali za maji zilizopo mipakani au maji yanayovuka mipaka ya nchi, lengo likiwa ni kuzuia migogoro, kukuza amani na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa maendeleo ya nchi.







No comments:
Post a Comment