
Shirika la umeme Tanzania ( TANESCO) limezindua rasmi zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wanaopisha mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa 220kV kutoka Masasi Mkoani Mtwara hadi Mahumbika Mkoani Lindi.

Akizungumza Mei 7, 2026 katika Kata ya Kiwalala, Halmashauri ya Mtama, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya umeme ikiwemo njia za kusafirisha umeme zitakazowezesha mikoa ya kusini kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa.
Amesema zaidi ya shilingi bilioni 5.1 zimetengwa kwa ajili ya kuwalipa takribani wananchi 1,730 katika mikoa ya Lindi na Mtwara watakaopisha mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa 220kV kutoka Masasi hadi Mahumbika
Bw. Twange, amesema kaya 78 katika vijiji vya Kiwalala na Mahumbika zitanufaika na zaidi ya shilingi milioni 253 katika awamu ya kwanza ya malipo kisha kuendelea katika vijiji vingine.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Victoria Mwanziva amesema ulipaji huo wa fidia unalenga kuhakikisha wananchi wote wanaopitiwa na mradi huo wanalipwa stahiki zao ili kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo hivyo amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa TANESCO
‘’Tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa kuidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 5.1 zitakazotumika kuwalipa fidia zaidi ya wananchi 1,700 katika maeneo ya Lindi na Mtwara lengo kuu ni kuhakikisha mradi wetu huu wa Masasi hadi Mahumbika unafanikiwa,’’alifafanua Mhe Mwanziva.
Zoezi hilo litaendelea katika vijiji vyote 46 vilivyoguswa na mradi huo katika Wilaya za Lindi, Ruangwa, Newala na Masasi.
Zoezi hilo la malipo linaanza kwa vijiji 14 vya Halmashauri ya Mtama.
Utekelezaji wa mradi huo utasaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi wa kusini, ambao kwa sasa wanategemea umeme unaozalishwa kupitia vituo vya gesi asilia vya Mtwara na kusafirishwa umbali mrefu.



No comments:
Post a Comment