MKENDA AITAKA MUST KUZALISHA WATAALAMU WA KUTEKELEZA MIRADI MIKUBWA YA TAIFA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, October 9, 2026

MKENDA AITAKA MUST KUZALISHA WATAALAMU WA KUTEKELEZA MIRADI MIKUBWA YA TAIFA



Na Mwandishi Wetu -
Mbeya




Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza zaidi katika sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuwawezesha wataalamu wa Kitanzania kutatua changamoto za wananchi na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo bila kutegemea zaidi wataalamu kutoka nje ya nchi.


Prof. Mkenda ameyasema hayo mkoani Mbeya wakati wa ziara yake katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), ambapo amekagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya chuo kupitia Mradi wa HEET, kutembelea bunifu za wanafunzi na watafiti pamoja na kufanya mazungumzo na uongozi wa chuo hicho.


Amesema vyuo vya sayansi na teknolojia vinapaswa kuelekeza nguvu katika tafiti na bunifu zinazolenga kutatua changamoto halisi za wananchi, huku vikihakikisha kuna mazingira wezeshi ya kuendeleza bunifu hizo hadi kuwa bidhaa na huduma zinazoweza kutumika nchini na kuuzwa katika masoko ya nje.


Prof. Mkenda amevitaka vyuo vya MUST, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo cha Nelson Mandela African Institute of Science and Technology kuandaa wataalamu wenye ujuzi na uwezo wa kubuni na kutekeleza miradi mikubwa ya kitaifa, hatua itakayosaidia kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje.

“Baada ya miaka 133 tangu reli ya kwanza ijengwe, bado tunapoamua kujenga reli tunatafuta watu kutoka nje. Lazima tujiulize, kwa nini tusiamini uwezo wa wahandisi wetu?” amesema Prof. Mkenda.

Amesisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kujiamini na kutumia uwezo wao katika sayansi, teknolojia na ubunifu, akirejea kauli ya marehemu Reginald Mengi isemayo, “Yes, we can, we will, we must,” kama hamasa ya kuamini uwezo wa ndani na kutafuta suluhisho la changamoto zinazolikabili taifa.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu, hususan vijana, ili mawazo na teknolojia wanazobuni ziweze kuendelezwa na kufikia hatua ya kuzalisha bidhaa na huduma zenye tija kwa jamii na uchumi wa taifa.

Amewapongeza wabunifu wa MUST kwa kuibua teknolojia mbalimbali zinazolenga kutatua changamoto za jamii, akieleza kuwa uwekezaji katika ubunifu utasaidia kuongeza uzalishaji wa ndani, kutengeneza ajira, kuongeza kipato cha wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania.










No comments:

Post a Comment